Jumatatu 21 Aprili 2025 - 09:44
Sifa za Imam: «‘Iṣmah»

Iwapo Imām hatokuwa ni mwenye kuhifadhiwa dhidi ya makosa, basi itawapasa watu wamtafute Imām mwingine ili awajibu mahitaji yao. Na iwapo na huyo pia hatokuwa ni mwenye kuhifadhiwa dhidi ya makosa, basi Imām mwingine atahitajika, na silsila hii itaendelea pasi na kikomo, na jambo kama hili, kwa mujibu wa akili ni batili.

Shirika la Habari la Hawza/ Mojawapo ya sifa muhimu za Imām na masharti ya msingi ya imāmah ni «iṣmah» (kuhifadhiwa dhidi ya maasi na makosa).

Iṣmah ni sifa thabiti inayozaliwa kutokana na elimu juu ya haki na ukweli, pamoja na irāda (azma) imara. Imām, kwa kuwa na vitu viwili hivi, hujiepusha kabisa na kutenda dhambi au kosa lolote.

Imām huwa ni mwenye kuhifadhiwa kutokana na makosa au dhambi yoyote, iwe katika kuelewa na kufafanua ma‘ārifa ya dini, au katika kuyatekeleza, au katika kutambua maslahi na madhara ya jamii ya kiislamu.

Kuhusu Iṣmah ya Imām, kuna dalili za kiakili na ki-naqli (kutoka katika Qur’ān na riwayah). Miongoni mwa hoja muhimu za kiakli ni hizi:

1. Hifadhi ya dini na mwenendo sahihi wa kidini, unategemea ismah ya Imām. Kwa kuwa Imām ndiye mwenye jukumu la kuilinda dini dhidi ya upotoshaji na kuwaongoza watu kidini, si tu kauli yake bali hata mwenendo wake, kukubali au kutokukubali kwake matendo ya wengine, huathiri mwenendo wa jamii. Hivyo basi, ni lazima awe ni mwenye kuhifadhiwa dhidi ya kila kosa katika kufahamu dini na kuifanyia kwazi, ili aweze kuwaongoza wafuasi wake kwa njia sahihi.

2. Sababu nyingine ambayo inaifanya jamii imuhitajie Imām ni hii kwamba,  watu katika kuifahamu na kutekeleza dini si wenye kuhifadhiwa na makosa. Sasa kama kiongozi wao naye pia si mwenye kuhifadhiwa na makosa, atawezaje kuwa mtu wa kuaminika kabisa kwao? Kwa maneno mengine, iwapo Imām si ma‘sūm, basi watu watakuwa na shaka katika kumfuata na kutekeleza maamrisho yake yote.

Zaidi ya hayo, iwapo Imām hatokuwa ni mwenye kuhifadhiwa dhidi ya makosa, basi italazimu kumtafuta Imām mwingine ili ajibu mahitaji ya watu. Na kama huyo naye si mwenye kuhifadhiwa na makosa, basi Imām mwingine atahitajika, na cheni hii itaendelea pasi na kuwa na kikomo, jambo ambalo kwa mujibu wa akili, ni batili.

Aya kadhaa za Qur’ān pia zinaashiria ulazima wa ismah kwa Imām, na mojawapo ya aya hizo ni āyah ya ۱۲۴ ya Sūrat al-Baqarah. Katika āyah hii tukufu, inasemwa kwamba baada ya makamu (cheo) cha Utume, Allah Mtukufu alimpa Hadhrat Ibrāhīm (‘alayhis-salām) cheo cha juu cha imāmah. Kisha Hadhrat Ibrāhīm (a.s) alimuomba Allah aendeleze cheo hicho kwenye kizazi chake pia.

Allah Mtukufu akasema:  

«لَا یَنَالُ عَهْدِی الظَّالِمِینَ.»  

“Ahadi yangu [ya Imāmah] haiwafikii madhalimu.”
Yaani, cheo cha imāmah ni maalumu kwa wale tu katika dhurriyya wa Ibrāhīm (a.s) ambao si madhalimu.

Sasa, kwa kuwa Qur’ān Tukufu inaona kwamba kumshirikisha Mwenyezi Mungu kuwa ni dhulma kubwa, na pia kosa lolote (yaani dhambi) limeitwa ni dhulma dhidi ya nafsi, basi yeyote aliyewahi kutenda dhambi katika kipindi chochote cha maisha yake, anakuwa miongoni mwa madhalimu na hastahili cheo cha imāmah.

Kwa ubainifu zaidi: Bila shaka, Hadhrat Ibrāhīm (‘alayhis-salām) hakuomba imāmah kwa ajili ya dhurriyya wake waliokuwa wakitenda dhambi katika maisha yao yote, au waliokuwa wema mwanzoni kisha wakawa waovu. Basi, kundi lililosalia ni mawili tu:

1. Wale waliokuwa waovu mwanzoni kisha wakatubu na kuwa wema.  
2. Wale ambao hawakuwahi kabisa kutenda dhambi katika maisha yao.

Mwenyezi Mungu, kwa kauli yake tukufu, amewatoa kwenye hesabu kundi la kwanza. Hivyo basi, cheo cha «Imāmah» ni maalumu kwa kundi la pili pekee.

Utafiti huu unaendelea...

"Imenukuliwa kutoka katika kitabu cha "Nagīni ya Afarinesh", pamoja na kufanyiwa mabadiliko kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha